Serikali  imeahidi kuendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazalendo katika utekelezaji wa miradi mikubwa lakini imewaonya wale ambao wamekuwa wakitekeleza miradi chini ya viwango vilivyowekwa kwenye mikataba.


Hayo yalisemwa jana mjini Dodoma na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, wakati akifungua mkutano wa mwaka wa makandarasi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB).

 

Samia aliagiza kuwa miradi yote ya thamani isiyozidi Sh bilioni 10 wapewe wakandarasi wa ndani hasa kwa miradi inayotekelezwa kwa fedha za ndani kwani wakandarasi hao watasaidia kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania na kuongeza uwekezaji ndani ya nchi.

 

Alisema kuwapa miradi mikubwa wakandarasi wazalendo kuna faida kubwa kwani kutasaidia kuwajengea uwezo hivyo kuweza kushindana na wakandarasi wa nje hivyo fedha nyingi za serikali kubaki ndani.

 

“Tanzania bora na yenye viwanda itatokana na wakandarasi bora na wenye uzalendo, hatuwezi kufikia huko tunakotaka kwenda wakati miradi mikubwa ya ujenzi inafanywa na wakandarasi wanje…. miradi ni yetu na fedha ni zetu hivyo lazima tuwape nyinyi,” alisema.

 

Aidha, aliwataka wakandarasi wazalendo wakamilishe kazi kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa pale wanapopewa miradi ili wajenge uaminifu kwa serikali kuendelea kuwaamini na kuwapa miradi mikubwa.

 

Makamu wa Rais aliwaonya baadhi ya wakandarasi wanaoshirikiana na maofisa wa serikali kuongeza gharama kubwa za ujenzi wa miradi kwa misingi ya rushwa hali ambayo imekuwa ikifuja fedha za serikali.

 

“Jamani kwenye mkutano huu tujitathimini na tuanze upya maana kuna wenzetu ambao hawana maadili na wanaendekeza rushwa, serikali ikitumia taasisi zake inatekeleza miradi mikubwa kwa gharama ndogo lakini nyinyi wengine mnaweka gharama kubwa ambazo si halisi,” alisisitiza.

 

Aliipongeza CRB kwa namna inavyoendelea kuratibu kazi za wakandarasi wazawa huku akiitaka kuendelea kuwajengea uwezo ili watekeleze miradi mikubwa kama kampuni ya nje.

 

“CRB mmefanyakazi kubwa sana kuandaa mkutano huu na kwa kuwa mmekutana hapa naomba mjadiliane kwa uwazi na muelezane ukweli kuhusu changamoto mlizonazo na namna mtakavyozitatua na sisi serikali mkituletea maazimio yetu sisi tunaahidi kuyafanyia kazi,” alisema.

 

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Mbarawa, yeye alisema asilimia 75 ya madeni ya wakandarasi yameshalipwa na yaliyobaki yatalipwa wakati ukifika na aliwaomba wawe wavumilivu wakati huu.

 

“Msidhani serikali imewasahau, tunafanya kazi kwa bidii kuhakikisha wote mnalipwa kwa sababu sisi tunaamini na tunafahamu kwamba ili makampuni yenu yaendelee lazima mlipwe hela zenu hivyo endeleeni kuchapa kazi hela zilizobaki zinakuja,” aliahidi Profesa Mbarawa.

 

Mwenyekiti wa CRB, Consolata Ngimbwa, aliomba serikali iharakishe malipo ya wakandarasi kwani wengi wao wako kwenye hali mbaya kifedha. Alisema baadhi ya wakandarasi walifariki dunia kutokana kabla hatajalipwa malimbikizo ya madeni wanayoidai serikali baada ya kukamilisha miradi mbalimbali ya ujenzi.

 

Alisema wakandarasi wengi wazalendo wana uwezo mkubwa wa kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi hivyo aliiomba serikali iweke kipaumbele kwa kuwapa miradi hiyo. 

 

Vile vile, aliwageukia wakandarasi ambao wamekuwa na kawaida ya kutekeleza miradi chini ya kiwango na wengine kutokomea mara baada ya kulipwa fedha za awali za ujenzi.

 

Msajili wa CRB, Rhoben Nkori aliwataka wakandarasi kutekeleza miradi wanayopewa na kuahidi kuwa bodi yake itaendelea kuhakikisha mkandarasi asiye na viwango anafutiwa usajili.

 

http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Joyce-10March2016.png

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo wa Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amesema uhakiki wa vyeti feki ulifanyika kwa umakini na kwa uhakika ili kutenda haki.

Ripoti iliyokabidhiwa kwa Rais John Magufuli na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela Kairuki, ilikuwa na orodha ya watumishi wa umma 9,932 walionainika kuwa na vyeti feki. Profesa Ndalichako alisema hadi kufikia kuwaweka wazi, ulifanyika uchunguzi wa kina na makini.

“Zoezi hili linafanyika kwa umakini na usahihi wa hali ya juu na zoezi hili la uhakiki limefanyika kwa mara ya kwanza tangu nchi ipate uhuru na limefanyika vizuri,” alieleza. Katika makabidhiano hayo mwishoni mwa juma mkoani Dodoma, Ndalichako aliwasisitiza kuwa uhakiki huo ni endelevu na kwamba huo wav yeti vya elimu utafuatiwa na vyeti vya kitaaluma.

Alisema baada ya uhakiki huo uliojikita katika vyeti vya kidato cha nne, kidato cha sita na ualimu, zamu inayofuata ni uhakiki wa vya kitaaluma baada ya kukamilika kwa uhakiki wa watumishi wa Serikali Kuu utakaotangazwa wiki hii.

Alisema Serikali imeziba njia zote za mkato katika elimu na ajira hivyo, vijana watumie muda walio nao kusaoma kwa bidii. Aliwataka waliojiunga katika vyuo vikuu bila sifa stahiki kuwajisalimishe ili kuepuka majuto ya baadaye.

Profesa Ndalichako alisema suala la kughushi vyeti vya taaluma na kutumia vya wengine limekuwa changamoto kubwa nchini. Alisema serikali imeziba njia zote za mkato kwenye elimu na ajira na kuwataka vijana wasome kwa bidii “Huwezi kujua ni lini utakamatwa na kuambiwa hauko kwenye njia zisizo sahihi, waliojiunga vyuo vikuu kwa njia ya mkato bora wajisalimishe wasipoteze muda na ili baadae wasije kujuta,” alisema Profesa Ndalichako na kuongeza kuwa serikali haina utani kwa watu walioghushi vyeti.

Alisema serikali ina dhamira ya kuhakikisha watumishi wenye sifa stahiki wanakuwepo kwenye utumishi wa umma na si vinginevyo na kwamba, Mei 5, mwaka huu Serikali itatoa taarifa ya uhakiki wa watumishi wa Serikali Kuu.

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ina mkakati wa kufanya Majiji yote nchini yawe na barabara za viwango vya kimataifa na zinazopitika kwa urahisi.

 

“Tumeanza kujenga barabara za kisasa katika jiji la Arusha ambalo ni jiji la utalii, tutakwenda Mwanza na Dar es Salaam kwa kujenga barabara zenye njia za juu (flyovers) zikiwemo za magari na za waenda kwa miguu,” amesema.

 

Ametoa kauli hiyo Alhamisi, Mei 4, 2017 wakati akizumngumza na wananchi wa Tengeru, wilayani Arumeru, mkoani Arusha mara baada ya kukagua barabara ya Sakina- Tengeru yenye urefu wa km. 14.1 ambayo itakuwa na njia nne za magari.

 

“Nimekuja kukagua ujenzi wa barabara hii ya Sakina hadi Tengeru lakini mkandarasi akimaliza anajenga barabara nyingine ya kilometa 42.1 na hivyo hapa Arusha tutakuwa na kilometa 56.5 za awamu ya kwanza,” alisema.

 

Alisema maboresho ya barabara za Jiji la Arusha yanafanyika ili kuwezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na viwanda vitakapoanza kujengwa, itakuwa hawana shida ya mawasiliano.

 

Akizungumzia tatizo la uhaba wa ardhi aambalo lililibuliwa na mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari, Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw, Mrisho Gambo aendelee na zoezi la kuuzungukia mkoa wake ili kubaini maeneo yenye matatizo sugu.

 

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo kwa Waziri Mkuu, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Eng. Mgeni Mwanga alisema ujenzi wa barabara hiyo ambao ulianza Juni 2015, unatarajia kukamilika Juni 2018.

 

“Ujenzi wa barara ya Sakina –Tengeru ni wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa km. 230 ya kutoka Arusha –Holili- Taveta –Voi ambayo ujenzi wake unatarajiwa kugharimu sh. bilioni 139.34. Ujenzi huo unagharimiwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

 

Sambamba na barabara hiyo, Eng. Mwanga alisema mkandarasi wa barabara hiyo ataanza kujenga barabara nyingine ya km. 42.1 inayoanzaia Usa River hadi Kisongo kwa kiwango cha lami ambayo itakuwa na madaraja saba wakati ile ya Sakina hadi Tengeru ina madaraja makubwa mawili.

 

Naye mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari alisems uhaba wa ardhi bado ni tatizo kubwa kwenye wilaya hiyo kiasi kwamba hawana hata eneo la kujenga shule au zahanati.

 

“Maeneo yote yameuzwa na wenyeviti wa vijiji na madiwani, hivi sasa ukitaka kujenga shule au zahanati hakuna eneo hata moja. Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba utusaidie kufuatilia suala hilo licha ya kuwa Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi alishakuja na kuelezwa hali halisi ilivyo,” alisema.

 

RAIS John Magufuli amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano zinalenga kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi na kujenga taifa linalomwamini Mungu.

Dk Magufuli aliyasema hayo mjini Moshi jana wakati alipoungana na waumini wa dini ya Kikristo kusali Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiaskofu, Jimbo Katoliki la Moshi, Parokia ya Kristo Mfalme na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na waumini wa makanisa hayo, aliwataka Watanzania kwa ujumla kuendeleza amani iliyopo nchini kwa kuwa ndio chachu ya maendeleo. “Napenda mniamini kuwa mimi nipo kwa niaba yenu, najua huu urais si wangu, urais mnao ninyi mlioamua nitumikie kama mtumishi kwa wakati huu, nawaomba sana muendelee kuniweka katika sala zenu ili kazi hii ya urais isinipe kiburi, nikawe mtumishi wa watu,” alisema Rais Magufuli.

Aliwashukuru waumini wa makanisa hayo mawili na Watanzania kwa ujumla kwa kusimama pamoja kuliombea Taifa amani iliyowezesha wananchi kupiga kura kwa amani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kutokana na sala zao Mwenyezi Mungu akamuwezesha kuwa Rais wa Tano wa Tanzania.

Pamoja na hayo, Dk Magufuli alitoa msaada wa mifuko 100 ya saruji kusaidia maendeleo ya Kanisa Katoliki na Sh milioni moja kwa kwaya ya kanisa hilo ili irekodi nyimbo zake. Akiwa KKKT, Rais huyo alitoa mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya kanisa hilo na Sh milioni moja kwa kwaya ya Kanisa hilo.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alimuunga mkono mkono Dk Magufuli kwa kuchangia mifuko 50 ya saruji na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki alichangia mifuko 50 ya saruji na Sh 500,000.

Kwa upande wa Askofu wa Jimbo la Katoliki la Moshi, Parokia ya Kristo Mfalme, Askofu Isaac Amani alimshukuru rais huyo kwa uamuzi wa kusali kanisani hapo na kuwataka waumini wa Kanisa hilo na Tanzania kwa ujumla kuendelea kumuomba Dk Magufuli na serikali yake awatumikie na kuwaletea maendeleo Watanzania.

Naye Askofu Mkuu wa KKKT, Askofu Dk Fredrick Shoo aliwataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kutokuwa na hofu kwa mambo yanayofanywa na rais huyo hususani katika kupambana na maovu, dhuluma na ufisadi na badala yake Watanzania wajenge mazoea ya kufanyakazi halali na kuwa waaminifu na wazalendo kwa taifa lao.

Aidha, Askofu Shoo alimuomba Dk Magufuli kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi hususani kwa taasisi za kidini zinazotoa huduma za kijamii zikiwemo zile za elimu na afya. Akijibu maombi hayo, Rais Magufuli aliwaeleza waumini na Watanzania kuwa serikali inathamini michango ya huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi za kidini na kuahidi kuliangalia suala hilo.

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Klabu ya Rotary nchini uangalie uwezekano wa kuisaidia Serikali kupambana na ugonjwa wa Malaria.

 

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye jana Alhamisi, Mei 4, 2017 alikuwa mwanachana wa 651 kujiunga na klabu hiyo,  alitoa wito huo wakati akifungua mkutano wa 92 wa mwaka wa Rotary unaojumuisha nchi za Uganda na Tanzania (District 9211) katika ukumbi wa AICC jijini Arusha.

 

"Ninatambua kazi nzuri inayofanywa na Rotary Club katika kuisaidia jamii kwa vile na mimi mwenyewe nimekuwa nikisaidia jamii. Kwa hiyo mimi na mke wangu Mary Majaliwa tunajiunga tukiwa ni wanachama wa 651 na 652 ili kuongeza nguvu ya Rotary kusaidia jamii," alisema huku akishangiliwa na washiriki zaidi ya 1,000 waliohudhuria mkutano huo kutoka Uganda, Tanzania, India, New Zealand na Australia.

 

Waziri Mkuu aliutaka uongozi wa klabu hiyo uongeze mikakati ya kutangaza kazi wanazozifanya ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa watu wengi kwamba wanaojiunga na klabu hiyo ni watu matajiri na watu maarufu.

 

"Kazi mnazozifanya ni kubwa na nzuri mno kwa jamii. Lakini itabidi mjitangaze zaidi ili watu wengi zaidi watambue kazi zenu na waweze kuwaunga mkono," alisema.

 

Waziri Mkuu aliahidi kuwashawishi viongozi wengine wa Serikali, taasisi za umma pamoja na Wabunge wajiunge kwa wingi na klabu hiyo. Tanzania ina klabu za Rotary 36 zenye wanachama 650 wakati Uganda ina klabu za Rotary 93 zenye wanachama 2,700. Tanzania na Uganda zinaunda District 9211 katika mfumo wa kimataifa wa rotary.

 

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapongeza wana-Rotary kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusaidia jamii hasa kwenye sekta za maji, elimu, na afya.

 

Alisema Rotary inatambulika duniani kwa kampeni yake ya kutokomeza ugonjwa wa polio; na kupitia michango ya wana-Rotary, Tanzania hivi sasa haina mgonjwa yeyote wa polio.

 

"Licha ya uchache wenu, natambua mchango mkubwa unaotolewa na Rotary Club hapa nchini. Hivi karibuni, Rotary Club saba ziliungana na Benki M na kujenga hospitali kubwa ya watoto pale Muhimbili (MNH) na Kituo cha Ujasiriamali kwa Vijana pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)," alisema.

 

"Miradi mingine inayofadhiliwa na Rotary Club ni ujenzi wa hospitali ya akinamama wajawazito mkoani Dodoma, utoaji wa vitabu vya ziada 20,000 kwenye shule za sekondari zaidi ya 40 mkoani Tanga pamoja na miradi ya maji safi kwenye  wilaya za Same na Mwanga mkoani Kilimanjaro.

 

Kwa upande wake, District Gavana wa Rotary 9211 ambaye anamaliza muda wake, Bw, Jayesh Asher wana-Rotary duniani wanaamini kwamba Serikali za nchi mbalimbali haziwezi kutekeleza majukumu yote kwa wananchi wake kwa hiyo wanajiunga na kutoa rasilmali zao ili kusaidia jamii zenye uhitaji.

 

Akizungumzia kuhusu uchahe wa wanachama hapa nchini, Bw. Asher alisema Rotary Club ya Uganda imepata umaarufu kwa sababu viongozi wengi wamejiunga na klabu hiyo wakiwemo Mawaziri, Spika wa Bunge la Uganda, wabunge na mabalozi.

 

“Hapa Tanzania itabidi tutangaze zaidi kazi zetu ili tuweze kuwavuta viongozi wa kisiasa na wa umma na pia kuongeza wanachama zaidi,” alisema.

 

Mkutano huo wa siku tatu, utamalizika Juni 6, mwaka huu.

 

Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe

SUALA la watumishi wa serikali 9,932 kuondolewa kazini kwa sababu ya kutumia vyeti feki, limetinga makanisani ambapo waathirika wa tukio hilo, wameambiwa wasijinyonge, kujidhuru au kujiua na badala wajipange upya kukabiliana na changamoto zilizopo mbele yao.

Akihuburi katika Kanisa la Kigango cha Dodoma-Makulu kilichopo katika Parokia ya Makole, Jimbo Kuu la Dodoma, Padri Yonah Mlewa alisema walioondolewa kazini wanatakiwa kutulia na kutafakari juu ya maisha yao, wasije wakafanya ujinga kujidhuru.

“Wafanyakazi hao waliondolewa kazini wanatakiwa kutulia na kutafakari, wasifanye ujinga wa kujidhuru au kujinyonga kutokana na kuondolewa huko kazini,” alisema Padri Mlewa na kuongeza kuwa waathika hao wanatakiwa kumtegemea Mungu katika kupanga cha kuendeleza maisha yao hasa katika kipindi hiki kigumu baada ya kuondolewa kazini.

Padri huyo aliyebobea katika masuala ya sheria, alisema lakini kama kweli wafanyakazi hao walipata ajira hiyo kwa kutumia vyeti feki, wanatakiwa kutubu na kuomba radhi kwa Mungu kutokana na kutumia vyeti feki hivyo.

“Ni kweli kutokana na kuondolewa kazini kwao, familia na wategemezi wao wengine wataathirika, lakini hiyo haiondoi ukweli kama waanyakazi hao walikuwa wakitumia vyeti feki,” aliongeza kiongozi huyo wa kidini.

Akionesha msisitizo, Padri Mlewa alisema wanatakiwa kukabiliana na maisha, kuomba mwongozo kwa Mungu baada ya kuondolewa, wakijua kwamba kufukuzwa kazi sio mwisho wa maisha, bali ni mwanzo wa hatua nyingine ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Aliwataka wafanyakazi hao ambao wengine ni waumini wa kanisa hilo, wasikate tamaa japo wameondolewa kazini, wanatakiwa kumtegemea Mungu kwani baada ya kufungwa mlango kazini walipokuwa wakifanya, mingine inaweza kufunguliwa na maisha yakaendelea.

Padri Mlewa alisema katika orodha hiyo kuna Wakristo wengi ambao wengine wanatumia hadi majina ya watakatifu, kama kweli walikuwa na vyeti feki wanatakiwa msamaha kutokana na kutumia vyeti feki.

“Kwa wale ambao wanajua kweli walikuwa wakitumia vyeti feki, hakuna lazima ya kukata rufaa, angekuwa yeye basi angeachana na rufaa akaondoka na kwenda kuanza kufanya kitu kingine,” alieleza Padri Mlewa.

Mmoja wa waumini katika kanisa hilo, Donath Kambanyuma alisema orodha hiyo ni ndefu na watu wengi wamekumbwa na kadhia hiyo, kinachotakiwa ni kujipanga upya na kuangalia mbele.

Mwishoni mwa wiki, Rais John Magufuli alipokea orodha ya watumishi wa serikali 9,932 kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, ambao wamejipatia ajira kwa vyeti vya kughushi.

Katika orodha hiyo, wafanyakazi wengi wanatoka katika halmashauri na wachache wanatoka katika taasisi nyingine za serikali yakiwamo mashirika ya umma. Katika hatua nyingine, Chama cha ACT -Wazalendo kinaunga mkono uamuzi wa serikali kuwachukulia hatua watumishi wote wa umma waliobainika kutumia vyeti feki ikiwemo kuwafukuza kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa chama hicho, Ado Shaibu, inabainisha kuwa bila shaka hatua hiyo itapanda mbegu ya uwajibikaji, kuchochea uadilifu na kuhakikisha uweledi kwenye utumishi wa umma.

“Mbali na kupongeza, yapo masuala kadhaa yaliyoibuka kwenye uhakiki huo ambayo tunadhani hayakwenda sawasawa na hivyo basi sisi kwa nafasi yetu tunao wajibu wa kuyakemea ili kuufanya mchakato huu uende kwa haki,” alieleza Shaibu.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kitendo cha Rais John Magufuli kuwasamehe wale watakaojiondosha kazini wenyewe na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale watakaoendelea kubaki kwenye nafasi zao jambo ambalo ni kinyume cha Sheria na Katiba ya nchi.

Alisema kisheria Rais hana mamlaka ya kumsamehe mtu anayetuhumiwa kufanya kosa la jinai iwapo mtu huyo hajafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa. “Madaraka pekee aliyonayo Rais ni kutoa Msamaha kwa wafungwa wanaotumikia kifungo kama alivyofanya hivi karibuni kwenye Sherehe za Muungano,” alisema.

Aidha, alitaja jambo jingine ambalo chama hicho hakikuridhika nalo kuwa ni madai ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, kuwa mchakato wa uhakiki wa vyeti haujawagusa wanasiasa na wateule wa rais kwa sababu cheti si sifa ya kupatikana kwao.

“Ikumbukwe kuwa msingi wa utaratibu huu ni kuhakikisha kuwa taifa linabaki na watumishi wenye sifa. Waziri Kairuki anasema kuwa sifa pekee ya Kikatiba ya Viongozi wa kisiasa ni kuwa wajue kusoma na kuandika.

Waziri hakutaka kujiuliza iwapo viongozi wa kisiasa watathibitika kughushi vyeti ambalo ni kosa la jinai haitawaondolea sifa yao ya uongozi? alihoji. Alimshauri waziri huyo mwenye dhamana ya utawala bora kuona kuwa uhakiki wa vyeti kwa viongozi wa kisiasa na wateule wa rais kama vile mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ni muhimu kwa kuwa unakwenda sambamba na viapo na matakwa ya kimaadili.

Wakati huo huo, ACT Wazalendo kinatarajia kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mei 5, mwaka huu, kikitimiza miaka mitatu tangu kilipopata usajili wa kudumu. Kwa mujibu wa Shaibu, maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Kahama mkoani Shinyanga.

“Kwa kuzingatia falsafa ya Mpango Mkakati wa Chama ya Siasa ni Maendeleo, maadhimisho ya miaka mitatu ya Chama yatajumuisha shughuli mbalimbali za kijamii kama vile usafi kwenye masoko ya mji na hospitali na kuwatembelea wafungwa,” alisema Mwenezi huyo. Alisema viongozi wa chama hicho wa kitaifa na Kahama watashiriki kwenye shughuli hizo

 

http://www.eatv.tv/sites/default/files/styles/detailpageimg/public/news/2017/05/01/Mgonjwa.jpg?itok=HJ5APcQL&timestamp=1493620690Mama mjamzito akisafirishwa kwa baiskeli kuelekea katika kituo cha afya. (Picha: Maktaba)

Shirika la mpango wa hifadhi ya jamii NSSF mkoa wa Ruvuma limetoa mifuko 800 ya Saruji na nondo kwaajili ya kujenga Zahanati ili kutatua tatizo la wananchi wa Kijiji cha Mhukuru Barabarani Songea wanaosafiri umbali mrefu kufuata huduma za matibabu.

Hatua hiyo itawawezesha wananchi wa kitongoji cha Matama kijiji cha Mhukuru Barabarani mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kujenga Zahanati kwakua tayari wamekwisha fyatua matofali elfu kumi na walikwama vifaa vya ujenzi vya vitendeakazi.

Kwa upande wao wananchi wa Mhukuru Barabarani hasa wanawake wameshukuru kwa hatua hiyo ya kupatiwa msaada huo ambao wamesema itasaidia kupunguza vifo vya wanawake na watoto.

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Songea Bw.Kuloleti Kamando Mgema amesema serikali inampango wakujenga Zahanati kila Kijiji ili kutatua tatizo la wananchi kupata huduma za matibabu.

Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.

RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) kitaifa. Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), sherehe hizo zitafanyika kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU).

Rais Magufuli aliwasili mjini Moshi juzi akitokea mkoani Dodoma na jana alishiriki Ibada za Jumapili katika makanisa mawili tofauti, na leo anatarajiwa kuongoza maelfu ya wakazi wa Moshi na miji jirani katika kilele cha sherehe hizo za Mei Mosi, huku wafanyakazi wakililia hali bora makazini.

Akizungumza wiki iliyopita, Katibu Mkuu wa Tucta, Yahaya Msigwa alisema, “Tayari tumemwandikia Rais Dk Magufuli kumuomba awe mgeni rasmi, kimsingi sherehe zote kitaifa mgeni rasmi ni yeye...tunazo ajenda za kumpa Rais, lakini moja ya mambo ambayo ni kero ni hili la mikataba ya hali bora kazini, wafanyakazi wengi wanafanya kazi kama vibarua na hawajui haki zao.”

Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Taifa lilipaswa kuwa na waajiriwa milioni 3.7 katika sekta iliyo rasmi, lakini waliopo ni 650,000 pekee hali inayoashiria kutokuwa na mikataba.

Alitolea mfano wa watumishi wa mashambani pekee nchini Kenya ni zaidi ya 700,000 na Afrika Kusini ni zaidi ya milioni moja na kwamba ipo haja kwa waajiri Tanzania kutafakari upya suala la maslahi ya wafanyakazi wao na rais anapaswa kulisemea hilo.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha Kampuni ya Synergy Tanzania Limited inayomiliki eneo la hekta 39 (ekari 96), mali ya Mbunge wa Jimbo la Kwimba, Shanif Mansoor inayodaiwa zaidi ya Sh milioni 500 za kodi ya ardhi, zinalipwa mara moja.

Lukuvi ametoa agizo hilo juzi jijini hapa wakati wa ziara yake ya siku mbili, baada ya kupokea taarifa ya kuwepo kwa watu wanaomiliki viwanja na hati na kushindwa kulipa kodi ya ardhi kwa wakati ikiwemo kampuni hiyo inayomilikiwa na mbunge huyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisikitika kuelezwa kuwa kampuni hiyo ilikwepa kulipa kodi hiyo ya ardhi tangu mwaka 2010 na kuuhoji uongozi wa Jiji la Mwanza ni kwanini ameshindwa kulipa kodi hiyo.

“Nilishasema mtu yeyote awe kiongozi, mbunge au mwanasiasa kwa Serikali ya Awamu ya Tano, hakuna exemption (msamaha wa kodi) na nilishasema wakati mnasimamia utozaji wa kodi msiangalie sura ya mtu, cheo chake au majina ya watu, kila mtu ni lazima alipe kodi,” alisema Lukuvi na kuongeza: “Akitaka suluhu, alipe kodi kabla ya Mei 5 mwaka huu, na akishindwa kufanya hivyo mpige mnada eneo hilo au nitampelekea Mheshimiwa Rais afute hati ya kumiliki eneo hilo.”

Ofisa Ardhi Mteule wa Jiji la Mwanza, Silvery Salavatory alisema halmashauri ilishindwa kutoa hati hizo kutokana na ukosefu wa vitendea kazi, wino, baadhi ya kompyuta kuharibika na makosa ya kibinadamu.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Mkoa wa Mwanza, Edward Masao alisema kampuni hiyo ya Synergy iliwasilisha pingamizi la kisheria lililoonesha kuwa kiwango cha madai ya fedha kilichokuwa kinadaiwa na halmashauri ni kikubwa kuliko uwezo wa baraza wa kuendesha shauri hilo.

 

Katika kuadhimisha Miaka 53 ya Muungano wa Tanzania tarehe 26 Aprili, 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

 

Wafungwa wote ambao baada ya punguzo la kawaida la moja ya tatu (1/3) linalotolewa chini ya Kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58, wawe wametumikia nusu (½) ya vifungo vyao vilivyobaki, isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2(i – xxi).

 

Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, Kifua kikuu (TB) na Saratani (Cancer) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa hawa wathibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

 

Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi. Umri huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

 

Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

 

Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability). Ulemavu huo uthibitishwe na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

 

Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

 

Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa.

Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

 

Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

 

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangik.

 

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji na upokeaji au utoaji rushwa.

 

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempt robbery).

 

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (fire arms, ammunitions and explosives).

 

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti au kujaribu kutenda makosa hayo.

 

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

 

Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki, uharibifu wa miundombinu au kujaribu kutenda makosa hayo.

 

Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).

 

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

 

Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mhe. Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

 

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

 

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

 

Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

 

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha kwa namna yoyote ile na nyara za Serikali na ujangili (poachers).

 

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

 

Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.

 

Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 16/03/2017.

 

Wafungwa warejeaji wa makosa/wafungwa waliowahi kufungwa gerezani (Recidivists).

 

Wafungwa 2,219 watafaidika na msamaha huu na wataachiliwa huru. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

 

 Meja Jenerali Projest Rwegasira

 KATIBU MKUU

WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

 

Subcategories

Call us:
(+255) 026-2782454
Address:
P.O.Box 1086, Chaungingi ST, Njombe, Tanzania.
Telephone: (+255) 026-2782454
E-mail: info@kingsfm.co.tz
Location      Contact Us