KATIKA kuadhimisha miaka 53 ya Muungano, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umewapongeza kwa dhati marais wote wastaafu huku wakimsifu Rais aliyepo madarakani, Dk John Magufuli kwa kuongoza nchi kwa busara na hekima na kuwa muumini wa kweli wa kuendeleza na kudumisha misingi ya Muungano.

Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumzia kuhusu maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano ambayo yataadhimishwa kesho mkoani Dodoma pamoja na kuwepo kwa mabadiliko ya kimuundo ndani ya UVCCM. Shaka alisema tangu kuapishwa kikatiba na kisheria kwa Rais Magufuli, amekuwa shupavu, mahiri ambaye hayumbi katika kuhakikisha hakuna kikundi au mtu anayegusa au kujaribu kuitikisa Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa Aprili 24, 1964.

Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM alisema katika aina au muundo na mfumo wa Muungano wowote lazima ziwepo changamoto, kujitokeza kwa kero mbalimbali na kuwa sehemu ya mchakato wa kuyafikia maendeleo kwa sababu yasiyokabiliana au kukumbwa na changamoto huwa si maendeleo halisi. Kuhusu mabadiliko ndani ya jumuiya hiyo, alisema katika kikao chake kilichofanyika Machi 12, 2017 mkoani Dodoma, ilipitisha mabadiliko ya 10 ya Kanuni ya UVCCM ikiwa ni kuwepo kwa wakuu wa Idara za Makao Makuu pamoja na utaratibu wa utumishi ndani ya jumuiya ili kuendana na matakwa ya Katiba ya Chama Cha Mapinduzi.

Alisema awali zilikuwepo idara nne za Makao Makuu na baada ya mabadiliko zimekuwa idara tano na baadhi ya idara zimepunguziwa vitengo na kuhamishiwa katika idara nyingine na baadhi ya wakuu wa idara waliokuwa wakishikilia nafasi hizo huku wakiteuliwa makatibu wa CCM wa wilaya hivyo kufanya kuwa wazi.

Shaka alisema katika mabadiliko hayo, uteuzi wa wakuu wa Idara za Makao Makuu zilikaimishwa ili kukamilisha muundo wa Kamati ya Utendaji ya UVCCM na walioteuliwa na idara wanazosimamia katika mabano ni Jokate Mwegelo (Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi), Dorice Obeid (Idara ya Uchumi, Uwezeshaji na Fedha), Daniel Zenda (Vyuo na Vyuo Vikuu), Mohamed Abdalla (Oganaizesheni, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa) na Israel Sostenes (Usalama na Maadili).

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amepongeza hatua zinazochukuliwa za kuboresha miundombinu na Serikali ya Awamu ya Tano na kubainisha kuwa katika miaka mitano ijayo, Tanzania inaweza kukua kiuchumi, kujenga viwanda vingi na kuongeza ajira. Profesa Lipumba aliyasema hayo wakati akihojiwa kwenye kipindi cha Jambo kinachorushwa na Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuhusu maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano yanayotarajiwa kuadhimishwa kesho.

Alisema ni jambo jema kwa Serikali ya Awamu ya Tano kuwekeza zaidi kwenye miundombinu kwani kwa kufanya hivyo, inaweza kukuza uchumi, lakini pia kuongeza ajira. “Kwa mfano kupitia bomba la mafuta kutoka Tanga kwenda Uganda hii itatoa fursa kwa Tanga kukua kiuchumi, hata uwekezaji wa viwanda na mashine za kusafisha mafuta unaweza ukafanyika,” alisema mwanasiasa huyo ambaye ni mchumi kitaaluma. Alisema mji wa Tanga una bandari na ardhi nzuri inayoweza kuzalisha kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo matunda, jambo litakalochochea uanzishwaji wa viwanda mbalimbali vitakavyotoa ajira kwa wananchi wa mji huo.

Pamoja na hayo, alibainisha kuwa Tanzania ina bahati ya kuwa bandari nyingi na kuzungukwa na nchi ambazo hazina bandari. Alitaja nchi kama vile Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi, Uganda na Rwanda kuwa zote hazina bandari hivyo ni fursa kwa Tanzania kutumia jiogrofia iliyopo kwa kujenga miundombinu mizuri na kujiunganisha na nchi hizo ili kuchochea ukuaji wake kiuchumi.

Akizungumzia manufaa ya Muungano, mwanasiasa huyo alibainisha kuwa manufaa makubwa hasa kwa upande wa utalii kwani kutokana na Muungano huo kwa sasa kuna fursa nzuri ya kujiingizia kipato na kuutangaza utalii huo. Hata hivyo, alisema pamoja kuwepo kwa fursa hiyo bado haijatumiwa vizuri kwani Tanzania kwa ujumla imebarikiwa kuwa na vivutio vya utalii vya kutosha zikiwemo mbuga mbalimbali za wanyama, Mlima Kilimanjaro na fukwe katika visiwa vya Zanzibar.

 

Call us:
(+255) 026-2782454
Address:
P.O.Box 1086, Chaungingi ST, Njombe, Tanzania.
Telephone: (+255) 026-2782454
E-mail: info@kingsfm.co.tz
Location      Contact Us