Kiongozi wa ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe

SUALA la watumishi wa serikali 9,932 kuondolewa kazini kwa sababu ya kutumia vyeti feki, limetinga makanisani ambapo waathirika wa tukio hilo, wameambiwa wasijinyonge, kujidhuru au kujiua na badala wajipange upya kukabiliana na changamoto zilizopo mbele yao.

Akihuburi katika Kanisa la Kigango cha Dodoma-Makulu kilichopo katika Parokia ya Makole, Jimbo Kuu la Dodoma, Padri Yonah Mlewa alisema walioondolewa kazini wanatakiwa kutulia na kutafakari juu ya maisha yao, wasije wakafanya ujinga kujidhuru.

“Wafanyakazi hao waliondolewa kazini wanatakiwa kutulia na kutafakari, wasifanye ujinga wa kujidhuru au kujinyonga kutokana na kuondolewa huko kazini,” alisema Padri Mlewa na kuongeza kuwa waathika hao wanatakiwa kumtegemea Mungu katika kupanga cha kuendeleza maisha yao hasa katika kipindi hiki kigumu baada ya kuondolewa kazini.

Padri huyo aliyebobea katika masuala ya sheria, alisema lakini kama kweli wafanyakazi hao walipata ajira hiyo kwa kutumia vyeti feki, wanatakiwa kutubu na kuomba radhi kwa Mungu kutokana na kutumia vyeti feki hivyo.

“Ni kweli kutokana na kuondolewa kazini kwao, familia na wategemezi wao wengine wataathirika, lakini hiyo haiondoi ukweli kama waanyakazi hao walikuwa wakitumia vyeti feki,” aliongeza kiongozi huyo wa kidini.

Akionesha msisitizo, Padri Mlewa alisema wanatakiwa kukabiliana na maisha, kuomba mwongozo kwa Mungu baada ya kuondolewa, wakijua kwamba kufukuzwa kazi sio mwisho wa maisha, bali ni mwanzo wa hatua nyingine ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Aliwataka wafanyakazi hao ambao wengine ni waumini wa kanisa hilo, wasikate tamaa japo wameondolewa kazini, wanatakiwa kumtegemea Mungu kwani baada ya kufungwa mlango kazini walipokuwa wakifanya, mingine inaweza kufunguliwa na maisha yakaendelea.

Padri Mlewa alisema katika orodha hiyo kuna Wakristo wengi ambao wengine wanatumia hadi majina ya watakatifu, kama kweli walikuwa na vyeti feki wanatakiwa msamaha kutokana na kutumia vyeti feki.

“Kwa wale ambao wanajua kweli walikuwa wakitumia vyeti feki, hakuna lazima ya kukata rufaa, angekuwa yeye basi angeachana na rufaa akaondoka na kwenda kuanza kufanya kitu kingine,” alieleza Padri Mlewa.

Mmoja wa waumini katika kanisa hilo, Donath Kambanyuma alisema orodha hiyo ni ndefu na watu wengi wamekumbwa na kadhia hiyo, kinachotakiwa ni kujipanga upya na kuangalia mbele.

Mwishoni mwa wiki, Rais John Magufuli alipokea orodha ya watumishi wa serikali 9,932 kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, ambao wamejipatia ajira kwa vyeti vya kughushi.

Katika orodha hiyo, wafanyakazi wengi wanatoka katika halmashauri na wachache wanatoka katika taasisi nyingine za serikali yakiwamo mashirika ya umma. Katika hatua nyingine, Chama cha ACT -Wazalendo kinaunga mkono uamuzi wa serikali kuwachukulia hatua watumishi wote wa umma waliobainika kutumia vyeti feki ikiwemo kuwafukuza kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa chama hicho, Ado Shaibu, inabainisha kuwa bila shaka hatua hiyo itapanda mbegu ya uwajibikaji, kuchochea uadilifu na kuhakikisha uweledi kwenye utumishi wa umma.

“Mbali na kupongeza, yapo masuala kadhaa yaliyoibuka kwenye uhakiki huo ambayo tunadhani hayakwenda sawasawa na hivyo basi sisi kwa nafasi yetu tunao wajibu wa kuyakemea ili kuufanya mchakato huu uende kwa haki,” alieleza Shaibu.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kitendo cha Rais John Magufuli kuwasamehe wale watakaojiondosha kazini wenyewe na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale watakaoendelea kubaki kwenye nafasi zao jambo ambalo ni kinyume cha Sheria na Katiba ya nchi.

Alisema kisheria Rais hana mamlaka ya kumsamehe mtu anayetuhumiwa kufanya kosa la jinai iwapo mtu huyo hajafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhukumiwa. “Madaraka pekee aliyonayo Rais ni kutoa Msamaha kwa wafungwa wanaotumikia kifungo kama alivyofanya hivi karibuni kwenye Sherehe za Muungano,” alisema.

Aidha, alitaja jambo jingine ambalo chama hicho hakikuridhika nalo kuwa ni madai ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, kuwa mchakato wa uhakiki wa vyeti haujawagusa wanasiasa na wateule wa rais kwa sababu cheti si sifa ya kupatikana kwao.

“Ikumbukwe kuwa msingi wa utaratibu huu ni kuhakikisha kuwa taifa linabaki na watumishi wenye sifa. Waziri Kairuki anasema kuwa sifa pekee ya Kikatiba ya Viongozi wa kisiasa ni kuwa wajue kusoma na kuandika.

Waziri hakutaka kujiuliza iwapo viongozi wa kisiasa watathibitika kughushi vyeti ambalo ni kosa la jinai haitawaondolea sifa yao ya uongozi? alihoji. Alimshauri waziri huyo mwenye dhamana ya utawala bora kuona kuwa uhakiki wa vyeti kwa viongozi wa kisiasa na wateule wa rais kama vile mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ni muhimu kwa kuwa unakwenda sambamba na viapo na matakwa ya kimaadili.

Wakati huo huo, ACT Wazalendo kinatarajia kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mei 5, mwaka huu, kikitimiza miaka mitatu tangu kilipopata usajili wa kudumu. Kwa mujibu wa Shaibu, maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Kahama mkoani Shinyanga.

“Kwa kuzingatia falsafa ya Mpango Mkakati wa Chama ya Siasa ni Maendeleo, maadhimisho ya miaka mitatu ya Chama yatajumuisha shughuli mbalimbali za kijamii kama vile usafi kwenye masoko ya mji na hospitali na kuwatembelea wafungwa,” alisema Mwenezi huyo. Alisema viongozi wa chama hicho wa kitaifa na Kahama watashiriki kwenye shughuli hizo

 

Call us:
(+255) 026-2782454
Address:
P.O.Box 1086, Chaungingi ST, Njombe, Tanzania.
Telephone: (+255) 026-2782454
E-mail: info@kingsfm.co.tz
Location      Contact Us