RAIS John Magufuli amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano zinalenga kuwaletea maendeleo ya kweli wananchi na kujenga taifa linalomwamini Mungu.

Dk Magufuli aliyasema hayo mjini Moshi jana wakati alipoungana na waumini wa dini ya Kikristo kusali Ibada ya Jumapili katika Kanisa la Kiaskofu, Jimbo Katoliki la Moshi, Parokia ya Kristo Mfalme na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza na waumini wa makanisa hayo, aliwataka Watanzania kwa ujumla kuendeleza amani iliyopo nchini kwa kuwa ndio chachu ya maendeleo. “Napenda mniamini kuwa mimi nipo kwa niaba yenu, najua huu urais si wangu, urais mnao ninyi mlioamua nitumikie kama mtumishi kwa wakati huu, nawaomba sana muendelee kuniweka katika sala zenu ili kazi hii ya urais isinipe kiburi, nikawe mtumishi wa watu,” alisema Rais Magufuli.

Aliwashukuru waumini wa makanisa hayo mawili na Watanzania kwa ujumla kwa kusimama pamoja kuliombea Taifa amani iliyowezesha wananchi kupiga kura kwa amani katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kutokana na sala zao Mwenyezi Mungu akamuwezesha kuwa Rais wa Tano wa Tanzania.

Pamoja na hayo, Dk Magufuli alitoa msaada wa mifuko 100 ya saruji kusaidia maendeleo ya Kanisa Katoliki na Sh milioni moja kwa kwaya ya kanisa hilo ili irekodi nyimbo zake. Akiwa KKKT, Rais huyo alitoa mifuko 150 ya saruji kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya kanisa hilo na Sh milioni moja kwa kwaya ya Kanisa hilo.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alimuunga mkono mkono Dk Magufuli kwa kuchangia mifuko 50 ya saruji na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadiki alichangia mifuko 50 ya saruji na Sh 500,000.

Kwa upande wa Askofu wa Jimbo la Katoliki la Moshi, Parokia ya Kristo Mfalme, Askofu Isaac Amani alimshukuru rais huyo kwa uamuzi wa kusali kanisani hapo na kuwataka waumini wa Kanisa hilo na Tanzania kwa ujumla kuendelea kumuomba Dk Magufuli na serikali yake awatumikie na kuwaletea maendeleo Watanzania.

Naye Askofu Mkuu wa KKKT, Askofu Dk Fredrick Shoo aliwataka waumini wa kanisa hilo na Watanzania kutokuwa na hofu kwa mambo yanayofanywa na rais huyo hususani katika kupambana na maovu, dhuluma na ufisadi na badala yake Watanzania wajenge mazoea ya kufanyakazi halali na kuwa waaminifu na wazalendo kwa taifa lao.

Aidha, Askofu Shoo alimuomba Dk Magufuli kuangalia uwezekano wa kupunguza kodi hususani kwa taasisi za kidini zinazotoa huduma za kijamii zikiwemo zile za elimu na afya. Akijibu maombi hayo, Rais Magufuli aliwaeleza waumini na Watanzania kuwa serikali inathamini michango ya huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi za kidini na kuahidi kuliangalia suala hilo.

 

Call us:
(+255) 026-2782454
Address:
P.O.Box 1086, Chaungingi ST, Njombe, Tanzania.
Telephone: (+255) 026-2782454
E-mail: info@kingsfm.co.tz
Location      Contact Us