Siku ya tatu ya ziara iliyofanywa na bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi nchini (TGDC) imekamilika ya kutembelea miradi ya kimkakati inayotekelezwa na kampuni hiyo mikoa ya Mbeya na Songwe, ambapo boodi hiyo iliambatana na uongozi wa TGDC.
Bodi hii ambayo ilizinduliwa mwishoni mwa mwezi wa saba mwaka huu, imefanya ziara yake ya kwanza na kujionea maendeleo ya miradi ya jotoradhi ambayo ni chanzo adhimu cha nishati ya uhakika, endelevu na rafiki wa mazingira.
Ziara hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Prof. Shubi S. Kaijage ambaye alifarijika na maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo yanayofanywa na TGDC ambayo ni Kampuni tanzu ya TANESCO, ambapo amesema
“Tumefarijika na maendeleo na jitihada zinazoendelea katika miradi ya jotoardhi, na tunaendelea kuishauri na kuielekeza Menejimenti ya TGDC ili tufikie malengo ya Megawati 200 ifikapo mwaka 2025 kama mipango mikakati ya Kampuni ilivyoainishwa na kutimiza malengo ya Serikali yetu”.
Kwa upande wa Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC Mhandisi Shakiru Idrissa amesema kuwa;
“Kazi ya kuchoronga visima vya jotoardhi itafanyika kwa kipindi cha miezi minne hadi sita kwa upande wa mradi wa Ngozi baada ya kufika Mtambo wa kuchoronga (drilling rig) unaotazamiwa kufika mwishoni mwezi ujao. Kampuni inategemea kupata Megawati 70 za awali kwa vipindi vya awamu mbili, awamu ya kwanza megati 30 na ya pili megawati 40 ifikapo mwaka 2025”.
Katika ziara hiyo Bodi ya Wakurugenzi ya TGDC ilifika katika mradi wa Kiejo-Mbaka uliopo Mbeya, ambapo TGDC imesha choronga visima vifupi vitatu vya utafiti huku kampuni ikitarajia kuzalisha Megawati 60 huku Songwe pekee ikitarajiwa kuzalisha Megawati 5 – 38.