Kuna uwezekano, changamoto ya mgao wa umeme ikabaki historia, baada ya kampuni ya uendelezaji jotoardhi Tanzania (TGDC) kuanza utekelezaji wa miradi mitano ya kipaumbele ya rasilimali joto ardhi ambayo itapatikana katika mikoa zaidi ya 16 nchini.

Kampuni hiyo ni kampuni tanzu ya Shirika la umeme #Tanesco ambapo inatekeleza nishati ya jotoardhi inayochimbwa urefu wa kilometa tatu kwenda chini na ina uwezo wa kuzalisha megawati 5,000 nchini.

Hayo yamesemwa leo Novemba 22 jijini Arusha na Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni ya TGDC , Mhandisi Shakiru Idrissa Kajugus wakati akizungumza katika ziara ya bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo ilipotembelea eneo la mradi lililipo Ziwa Natron wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.

Amesema kuwa,nishati hiyo ya jotoardhi inapatikana kwa wingi katika maeneo ya bonde la Ufa ambapo kwa upande wa Ziwa Natron wapo katika hatua za utafiti kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utazalisha megawati 60 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2025 .

“Mradi huu wa Ziwa Natron kwa kuanzia tutazalisha megawati 10 baada ya hapo tunaendelea na upanuzi zaidi na unatarajiwa kugharimu kiasi cha zaidi ya shs 1 bilioni na kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa sana kwa wananchi kwani ni nishati endelevu ya kisasa isiyotegemea mabadiliko ya tabia ya nchi. “amesema Mhandisi Kajugus.

Ameongeza kuwa,Tanzania kwa sasa tuanatekeleza miradi miatano ya kipaumbele na huo huo ni mmojawapo, maeneo hayo yapo; Mkoa wa Mbeya ipo miradi miwili katika wilaya ya Rungwe katika maeneo ya Ngozi na Kiejo – Mbaka huku mikoa mingine ikiwa ni Songwe na Pwani na tayari ipo katika hatua ya uhakiki kwa ajili ya kuchimba visima huku kwa mkoa wa Arusha wakiendelea na tafiti za kisayansi ambazo zinatarajiwa kumalizika mwaka 2023.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya TGDC ,Profesa Shubi Kaijage amesema kuwa; ikiwa kama bodi mpya wamefikia hatua ya kutembelea moja ya miradi ya kampuni hiyo kujionea na kuweza kuangalia cha kushauri ili mradi huo uweze kufanyiwa kazi kwa haraka na kwa weledi.

Amesema kuwa, nishati hiyo inapatikana chini ya ardhi kwa kutumia joto lililopo chini ya ardhi na kuwa itaweza kupunguza sana changamoto ya mgao wa umeme uliopo hivi sasa unaosababishwa na ukame.Kwani nishati hii ni endelevi na haiathiriwi na mabadiliko ya tabia nchi.

“Sisi kama bodi tunaendelea kuhakikisha tunasimamia kikamilifu mradi huu ili uweze kukamilika kwa wakati ,na tunaomba kampuni hii iendelee kutekeleza majukumu yake kwa wakati ili tuendelee kupata vyanzo zaidi vya umeme .

X