Na Imani Henrick
“Nilichokifanya niliacha tu kwa muda kidogo (kutumia Instagram) halafu nikaendelea ili kuaminisha watu kwamba sioni aibu kwa kile kilichotokea kwa sababu ilikua ni kitu cha kutengenezwa,”
Huyu ni Amida Twaha ambaye miaka mitatu iliyopita alipitia unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni akiwa mwaka wa pili akisoma stashahada katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), jambo ambalo kwa wakati huo lilihatarisha elimu na maisha yake.
Siku moja alipoamka na kushika simu yake ili kuperuzi kwenye mtandao wa kijamii, ghafla akakutana na mjadala mkali katika moja ya kundi sogozi la WhatsApp ambalo yuko na wanafunzi wenzake. Walikuwa wakimjadili huku wengi wao wakimtukana na kumpatia kila maneno mabaya baada ya mmoja wa marafiki zake kusambaza kipande cha video kilichokuwa kinamuonesha akiwa mtupu.
Siku hiyo ilikuwa moja ya siku mbaya kwa Amida (20) kwa sababu wanafunzi wenzake hata marafiki wa karibu walimuona hafai na pia mtu asiye na maadili kwa video ya utupu ambayo alijirekodi mwenyewe.
Amida anasema mtu aliyevujisha video hiyo alikusudia kumuharibia sifa yake njema katika jamii ya wanachuo kutokana na mafanikio aliyokuwa ameyapata katika tasnia ya urembo ikiwemo kushinda taji la ulimbwende chuoni MUST mwaka 2019.
“Unajua kwenye haya mashindano kunakua na mtu anampenda mtu fulani ashinde, kwa hiyo mtu akishakuona labda wewe una uwezo mkubwa, anaona labda utamshinda mtu wake, kinachotokea pale ni mtu anaweza akakubully (akakudhalilisha) kama vile ilivotokea kwangu,” anasema Amida.
Baada ya tukio hilo, kutokea alitoa taarifa kituo cha Polisi lakini kesi yake haikushughulikiwa kama vile alivyotarajia na hata mtuhumiwa hakuchukuliwa hatua zozote.
Licha ya ukatili huo aliofanyiwa, ilimchukua muda mfupi binti huyo kurejea katika hali ya kawaida na masomo kwa sababu alipata ushauri nasaha. Hata yeye anakiri kwamba bila kuchukua hatua hiyo, huenda ingekuwa ngumu kurejea kwenye hali ya kawaida kama ilivyo kwa watu wengine ambao wanakutana unyanyasaji kama huo wakakosa huduma hii.
“Nilivyorudi chuo wakaniuliza kama ninaweza kuendelea na masomo au wanihamishie chuo kingine lakini nilichagua kuendelea hapo hapo kwa sababu kutatua tatizo sio kukimbia tatizo.” anasema Amida, na kuongeza kuwa “Nilihisi nikienda chuo kingine watu wataanza kunishangaa lakini hawa walionizoea watakua tu na shauku ya kuniona kama kweli ni mimi,”
Hata hivyo, Amida anakiri kuwa uamuzi wake haukuwa mwepesi kwa sababu wakati mwingine alikuwa akinyooshewa vidole na wanafunzi wenzake lakini kama alivyojifunza kwenye ushauri nasaha, baadaye hali ilitulia.
Anasema Hakuacha kupigania ndoto yake ya urembo na hivyo aliendelea kushiriki mashindano mbalimbali ya ulimbwende ikiwemo kushindania Ulimbwende wa Nyanda za Juu Kusini na baadaye Miss Tanzania ambapo alifikia hatua ya 20 bora.
Amida ni miongoni mwa wasichana na wanawake Tanzania na duniani wanaokumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia mtandaoni hasa wapotumia mitandao ya kijamii.
Hali hiyo huwanyima haki na uhuru wa kujieleza, kuwakosesha fursa kuwasiliana, kuzoretesha mahusiano na kuwanyima fursa mbalimbali za mtandaoni ikiwemo mafunzo na biashara.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mtaifa (UN) ya mwaka 2016 kuhusu namna ukatili wa kijinsia wa mtandaoni unavyoathiri haki za binadamu, asilimia 70 ya vijana (au vijana saba kati ya 10) wamewahi kupitia ukatili wa kijinsia wakati wanatumia intaneti duniani.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mhanga mmoja kati ya watatu wa ukatili huo amejidhuru ikiwemo kujaribu kujiua kama njia ya kutatua tatizo.
Kimsingi ukatili wa kijinsia wa mtandaoni ni unyanyasaji unaotendeka kwa kutumia teknolojia za kidijitali. Mtu anaweza kufanyiwa ukatili huu kwenye mitandao ya kijamii, majukwaa ya kutuma ujumbe, michezo ya kubahatisha na hata kwenye simu za mkononi.
Ukatili huu huwa na tabia ya kujirudia, lengo likiwa ni kutisha, kukasirisha au kuwaaibisha wale wanaolengwa.
Mifano ya matendo ya ukatili wa kijinsia wa mtandaoni ni pamoja na kueneza uwongo, na hata kutuma picha au video za aibu za mtu fulani kwenye mitandao ya kijamii.
Pia wahalifu hutumia ujumbe, picha au video za kuumiza, matusi au vitisho kupitia mifumo ya ujumbe na kutuma ujumbe mbaya kwa wengine kwa niaba yao au kupitia akaunti za kughushi.
Wanawake wako katika hatari zaidi
Licha ya kuwa ukatili huwapata wanawake na wanaume, lakini ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa wasichana na wanawake ndiyo wanakumbana zaidi na vitendo vya ukatili mtandaoni ukilinganisha na wanaume.
Taasisi ya kimataifa ya Sera Bora kwa Maisha Bora (OECD) katika moja ya andiko lake kuhusu maisha katika zama za kidijitali la mwaka 2019, inaeleza kuwa wasichana wanapata ukatili wa kijinsia mtandaoni mara mbili zaidi ya wenzao wa kiume.
Kuongezeka kwa vitendo vya ukatili wa mtandaoni kwa wanawake kunachangiwa kwa sehemu kubwa na ukosefu wa elimu ya matumizi sahihi ya intaneti na kutawala kwa mfumo dume ambao wahalifu huuendeleza hadi mtandaoni ili kushusha hadhi ya kundi hilo muhimu kwenye jamii.
Baadhi ya wadau wa masuala ya haki za binadamu nchini Tanzania wanaeleza kuwa kuongezeka kwa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia mtandaoni, kunachangiwa na kutokuwepo kwa elimu ya kutosha na usimamizi mzuri wa sheria zinazohusu matumizi salama ya mitandao ya kijamii kama anavyoeleza Ibrahim Chawe, mkazi wa jijini Dar es Salaam.
“Kuhusu sheria sijui sana, najua tu juu juu kwamba ukifanya cyberbullying (unyanyasaji mtandaoni) ni kosa kisheria kwa maana unaweza ukakamatwa au ukafungwa, mambo ya faini sijajua lakini najua kwamba ni kosa kisheria.
“Kwa hiyo kutokana na uelewa wangu mdogo naweza nikasema kwamba hizo sheria hazitekelezwi vizuri. Mamalaka zina wajibu wa kuhakikisha watu wanazielewa hizo sheria lakini vile vile wahusika wanaofanya vitendo vya ukatili mtandaoni wachukuliwe hatua za kisheria,” anasema Chawe.
Utafiti kuhusu unyanyasaji wa kijinsia wa mtandaoni kwa wanawake wanaoshiriki siasa Tanzania wa mwaka 2021 uliofanywa na taasisi zaidi ya nne ikiwemo Media Convergency na Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) unaeleza kuwa hakuna taarifa na takwimu za kutosha kuhusu ukatili huo nchini huku kukiwa hakuna sheria maalum kusimamia suala hilo.
Sheria zinazoshughulikia suala hilo
Kwa sasa, ukatili huo unashughulikiwa na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka
2015. Sheria hiyo inakataza vitendo vya udukuzi wa mitandaoni, uonevu na matusi yanayochochewa na ubaguzi wa rangi na chuki ili kuwalinda watumiaji wa mtandao.
Licha ya kukosekana kwa sheria moja na ya kina ya kuwalinda watu dhidi ya ukatili wa kijinsia mtandaoni, hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 nazo zinakataza matendo yoyote yaliyo kinyume na haki za wanawake ikiwemo yale yanayotendwa mtandaoni.
Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015, mtu atakayefanya ukatili wa kijinsia mtandaoni anaweza kukabiliwa na adhabu ya faini ya Sh5 milioni au kifungo kisichopungua miaka 3 au vyote kwa pamoja.
Kama ilivyo kwa aina nyingine za ukatili, ukatili wa mitandaoni una madhara mbalimbali ikiwemo kusababisha msongo wa mawazo, kumpotezea mwanamke mwelekeo katika Maisha na hata kujiua.
Pia unajenga hofu na kuvunja moyo wanawake kushiriki kwenye shughuli za kijamii, ngazi za uongozi na maamuzi wakihofia kudhalilishwa na kutwezwa utu wao.
Ripoti ya utafiti wa uhuru wa kuwa mtandaoni wa Shirika la kimataifa linaloshughulikia masuala ya watoto na wasichana la Plan International ya mwaka 2020 inaeleza kuwa ukatili wa mtandaoni umechangia asilimia 19 ya wasichana duniani kupunguza au kuacha kabisa kutumia mitandao ya kijamii huku asilimia 12 wakibadilisha namna ya kuwasilisha mawazo yao wanapokuwa mtandaoni.
Hali hiyo inachangia kuwafanya wasichana kutokuwa na nguvu katika ulimwengu wa kidijitali na kuathiri uwezo wao wa kuonekana, kusikilizwa na kutumia vizuri fursa za mtandaoni.
Utafiti huo uliowashirikisha wasichana na wanawake 14,000 wenye umri kati ya miaka 15 hadi 25 kwenye nchi 22, ikiwemo Brazil, Benin, Marekani, Nigeria, Uhispania, Thailand na India unaeleza kuwa zaidi ya nusu au asilimia 58 ya wasichana wamewahi kukumbana na ukatili wa mtandaoni.
Wakati utafiti huo ukieleza namna ukatili wa kijinsia unavyoathiri wanawake wanaotumia mitandao ya kijamii, Amida hakuacha kutumia mitandao ya kijamii. Alifungua akaunti nyingine ya Instagram ambapo anaitumia kutoa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia ili kuwalinda wasichana wenzake dhidi ya vitendo hivyo kupitia mradi wake wa “Zuia Ukatili wa Kijinsia Mtandaoni na Eneza Upendo Mtandaoni.”
Ufanye nini ukifanyiwa ukatili mtandaoni?
Ikiwa umefanyiwa ukatili wa kijinsia unatakiwa kufanya nini ili upate msaada? Umoja wa Mataifa (UN) katika moja ya maandiko yake kuhusu ukatili wa kijinsia unaeleza kuwa ni muhimu kwa wahanga wa ukatili huu kutokukaa kimya wafanyiwapo uonevu mtandaoni.
Hatua ya kwanza ni kutafuta msaada kutoka kwa mtu unayemuamini kama vile wazazi, rafiki, mwanafamilia au mtu mzima mwingine unayemuamini. Ikiwa uko shuleni au chuoni unaweza kuwasiliana na mshauri au mwalimu unayempenda na unaweza kufanya hivi kwa njia ya mtandao au ana kwa ana.
Ikiwa uonevu unafanyika kwenye mtandao wa kijamii, toa taarifa kwa wamiliki wa mtandao husika kuhusu udhalilishaji uliofanyiwa ili akaunti ya muhusika isimamishwe kuzuia kusambaa kwa maudhui mabaya dhidi yako.
Hatua nyingine ni kukusanya na kuhifadhi ushahidi, iwe ni ujumbe mfupi au picha za simu ili kuonyesha kile ambacho kimekuwa kikiendelea.
Ikiwa uko katika hatari na unahitaji jambo hilo kutatuliwa kwa dharura basi unapaswa kuwasiliana na polisi au huduma za dharura katika eneo lako.
Hatua zinazochukuliwa kukomesha ukatili huo
Mkurugenzi wa taasisi ya Media Convergency Asha Abinallah anasema wadau wa masuala teknolojia na jinsia Tanzania wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu suala hilo kwa kuunganisha nguvu ili kumlinda mtoto wa kike anapokuwa mtandaoni.
“Tunafanya kazi karibu na waandishi, tena waandishi wanawake na wakati mwingine wanaume tunakaa nao na kuongea juu ya hii ajenda kwa sababu moja ya kitu ambacho tumegundua ni kwamba hakuna taarifa nyingi zilizoandikwa kuhusiana na unyanyasaji wa mitandaoni,” anasema Asha ambaye taasisi yake inasimamia mradi wa “Women at Web” unaowasaidia wanawake kutumia mitandao vizuri na kukabiliana na ukatili wa kijinsia mtandaoni.
“Tunawapa nyenzo juu ya namna ya kutumia mitandao ya kijamii, jinsi ya kuwa waandishi wazuri wa dijitali. Pia tunawafikia wanafunzi wa vyuo wale ambao ni viongozi na wengine ambao wanaweza kuwafikia wengine kwa sababu wanavyuo wamekua wahanga wa unyanyasaji mtandaoni ikiwemo uvujishwaji wa picha zao za utupu,”anasisitiza mtaalam huyo wa masuala ya teknolojia.
Asha anasema taasisi yake inashirikiana na wadau muhimu kama polisi, mashirika yasiyo ya kiserikali yanoshikilia agenda za unyanyasaji wa kijinsia na kuchagiza uanzishwaji sharia maalum kushughulikia aina hiyo ya ukatili.
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Njombe, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Wilfred Willa anasema ili kukomesha ukatili wa kijinsia unaotokea mtandaoni ni watu kuvunja ukimya na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili wanaotenda vitendo hivyo wachukuliwe hatua za kisheria.
“Nisisitize tu kwamba wewe muhanga njoo polisi njoo dawati tuzungumze tufungue kesi ili haki yako uipate, kwa sababu usipokuja watu hao wataendelea kufanya matendo haya kwa watu wengine na kwako pia, mwisho wa siku tutakua na kizazi ambacho kina makosa mengi sana ya ukatili kwa njia ya mtandao,” anasema Willa.
Willa anaeleza kuwa jamii pia inapaswa kuwa mstari wa mbele dhidi ya matukio hayo na kuwa tayari kutoa ushahidi mahakamani pale mtumuhumiwa anapofikishwa kizimbani.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa taasisi ya Media Convergency, Asha Abinallah anasema ili kupata suluhu ya kudumu dhidi ya ukatili huo uboresha wa sheria zinazosimamia matumizi ya mitandao ya kijamii ufanyike na kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi na kuwahusisha watunga sera katika mapambano hayo.